Share:

Daz Baba: Singeli waachiwe vijana, wakongwe tuendelee na harakati zetu

Msanii mkongwe wa muziki aliyewahi kufanya vizuri na wimbo ‘Namba 8’ Daz Baba amewataka wasanii wenzake wakongwe kutothubutu kuiga muziki wa vijana wapya.

Rapper huyo ambaye anajipanga kuachia kazi mpya hivi karibuni, ameiambia Bongo5 kuwa wasanii wakongwe wanatakiwa kuendelea kufanya muziki ambao uliwatambulisha kwenye game.

“Mimi binafsi sikati tamaa kwa sababu bado naendelea kufanya muziki wangu ambao nilikuwa naufanya toka nyuma, kwa hiyo bado nina mashabiki wa muziki wangu,” alisema Daz “Watu wanatakiwa kujua kila kizazi kina wasanii wake na muziki wake, ukirudi nyuma kidogo tupo sisi, akina Soggy, Afande Sele na wengine, wapo wa muziki wa Singeli, wapo akina Ali Kiba na Diamond, kwa hiyo ukinikuta mimi naingia kwenye muziki mwingine nitakuwa nawakosea mashabiki wangu,”

Aliongeza, “Vinaja waachwe wafanye muziki wao, kama ni Singeli au muziki gani, na sisi wakongwe tuendele na muziki wetu wa harakati kwa sababu kuna watu wetu tumetoka nao kule nyuma na bado wanatupenda,”

Daz amewataka mashabiki wake kuendelea kukaa mkao wa kula kwa ajili ya wimbo wake mpya ambao utatoka wiki ijayo.